Maximo atuma salamu kwa wapinzani wake mapema

Kocha mkuu wa kikosi cha Dar es salaam Young Africans, Marcio Maximo ametangaza hali ya hatari kwa timu zitakazoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa mwaka 2014-15.

Akizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo, Jangwani, jijini Dar es Salaam, Maximo amesema hana budi kutuma salamu mapema kwa wapinznai wake kutokana na maandalizi kabambe anayoendelea kuyatoa kwa wachezaji wake hususan walipokuwa kisiwani Zanzibar.
Pamoja na kuwasilisha salamu wa kuwataka wapinzani katika ligi kuu wakae tayari kupokea dozi kutoka kwenye kikosi chake, kocha huyo ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, ameonyesha kuihofia ratiba ya ligi iliyotolewa juma lililopita kwa kusema ni ngumu katika michezo ya awali, lakini bado kasisitiza kutohofia chochote zaidi ya kuamini kikosi chake kipo vizuri.
Katika hatua nyingine Maximo amesema kabla ya kucheza mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Azam FC mnamo Septemba 13, kikosi chake kitacheza michezo miwili ya kujipima nguvu siku ya Jumatano na Jumapili na kwamba ataendelea na utamaduni wa kutoa nafasi kwa wachezaji wote kucheza.
Maximo amesema ana matumaini makubwa michezo hiyo ya kirafiki itakisaidia kikosi chake kujiimarisha kuelekea msimu mpya, wakianza na mchezo wa Ngao ya Jamii.
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi wakianza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Popular Posts