HII NDIO E-CIGARETTE ,SIGARA YA KIELECTRONIKI ISIYOTUMIA TUMBAKU
Wakati dunia ikiendelea na vita dhidi ya uvutaji sigara, wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Auckland, New Zealand, wamegundua teknolojia mpya ya sigara ya kieletroniki (E-cigarettes), ambayo
inawasaidia wavutaji kuacha na wengine kupunguza uvutaji kwa asilimia zaidi ya 50.
Chuo Kikuu cha Auckland kilichoanzishwa mwaka
1883, kinaheshimika kwa kutoa wanataaluma wenye weledi, kina wanafunzi
kutoka zaidi ya nchi 90 na mwaka 2011 kilishika nafasi ya 82 ya vyuo
bora duniani, kwa maana hiyo utafiti wake umekuwa hautiliwi shaka.
Kutokana na heshima yake kitaaluma, wanasayansi wa
chuo hicho hivi karibuni wamefanikiwa kugundua kifaa kinachotumia
betri, chenye nikotini ambayo siyo halisi, mtumiaji anapovuta sigara
hiyo hupata faida ya kuacha au kupunguza kwa asilimia kubwa matumizi ya
tumbaku.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa chuo hicho
umegundua kuwa, licha ya kuwepo plasta zilizo na nikotini (sumu iliyo
kwenye tumbaku), kwa ajili ya kumsaidia mvutaji kuacha, teknolojia ya
sigara ya kielektroniki imeonekana kukubalika kwa watumiaji wengi.
Vichwa vya wanasayansi vimekuwa vikiumia kila
kukicha kusaidia jamii kuondokana na matumizi ya tumbaku yenye madhara
kiafya kwenye mwili wa mwanadamu.
Mfano, takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya
Duniani (WHO) zinaonyesha takribani watu milioni sita hufa kila mwaka
kutokana na matumizi ya tumbaku na zaidi ya watu 600,000 hufa kutokana
na kuvuta moshi wa mtu anayevuta.
Kumekuwapo na juhudi nyingi za kuhamasisha jamii
kuacha kutumia tumbaku. Kwa mfano mwaka juzi Serikali ya Marekani
ilitangaza kuzindua kampeni iliyogharimu dola 54 milioni kupitia
matangazo ya kibiashara yaliyolenga kuelimisha umma madhara ya uvutaji
sigara.
Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa ya Marekani (CDC),
ndiyo iliyoratibu matangazo hayo ya kibiashara kwenye redio,
televisheni na mitandao ya kijamii pamoja na mabango katika muda wa
miezi mitatu.
Mfano wa tangazo mojawapo la kibiashara
linaonyesha mwanamume wa miaka 31, ambaye amekatwa miguu yote miwili
baada ya kupata ugonjwa unaoathiri damu, unaosababishwa na uvutaji
sigara, lengo ni kuamsha uelewa wa watu kuhusu ubaya wa sigara.
Kugunduliwa kwa sigara hiyo ya kielektroniki
huenda ukawa ni msaada mwingine kwa wanaotaka kuacha uvutaji wa sigara,
lakini wanashindwa kwa hiari yao hadi wapate kichocheo cha kuwalazimu
kufanya hivyo.www.pallangyo,blogspot.com
Sigara hiyo ya kielektroniki mwonekano wake ni
kama sigara halisi na huibadili nikotini iliyowekwa ndani yake kuwa ya
unyevunyevu, pale mtumiaji anapoivuta.
Wanasayansi hao bado hawajathibitisha kiwango cha
madhara ya ndani ya nikotini iliyomo kwenye sigara hiyo, lakini
imeelezwa kuwa na madhara kama sigara zingine halisi. CHANZO MWANANCHI NEWS PAPER TANZANIA by NOOR SHIJA