MTOTO AMUUA MWALIMU KWA BUNDUKI KATIKA AJALI
Msichana wa miaka tisa nchini Marekani amemuua kwa kumpiga risasi, kwa bahati mbaya, mwalimu wake aliyekuwa akimfundisha jinsi ya kutumia bunduki.
Mwalimu huyo alikuwa akimpa mafunzo msichana huyo katika kituo cha kupigia risasi kilichopo Arizona, wakati msichana huyo alipopoteza mwelekeo baada ya kufyatua risasi ya kwanza, katika bunduki aina ya Uzi.
Mwalimu huyo, Charles Vacca, 39, alipigwa risasi kichwani na kufariki wakati akipelekwa hospitali kwa ndege mjini Las Vegas.
Msichana huyo alikuwa katika kituo hicho pamoja na wazazi wake.
Ajali hiyo ilitokea Jumatatu iliyopita katika kituo cha kupiga risasi cha Last Stop, kilichopo White Hills, Arizona.
Waandishi wa habari wanasema ni jambo la kawaida katika maeneo mengi nchini Marekani kwa watoto kufunzwa jinsi ya kutumia bunduki.
Vituo vingi vya kupigia risasi huwa vina sheria kali za usalama hasa kwa watoto. Haifahamiki kituo hicho kina kanuni zipi kuhusiana na umri wa chini ambao watoto wanaruhusiwa kuanza mafunzo.