Ofisi ya Bunge yatoa ufafanuzi kuhusu malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
Mkurugenzi
wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey Mwakasyuka (kushoto) akitoa ufafanuzi
mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na malipo ya
posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba katika ukumbi wa mikutano
ofisi ya Bunge mjini Dodoma
OFISI
ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa
zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya
posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Ufafanuzi
huo umetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Itifaki Bw. Jossey Mwakasiyuka
wakati alopokutana na waandishi wa habari kwa lengo la kutolea
ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo zilizoikera ofisi hiyo ya Bunge
Maalum.
Mwakasyuka
amevieleza vyombo vya habari kuwa, ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na
kuchapishwa kwa taarifa hizo na baadhi ya vyombo vya habari kwani
taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha
Waheshimiwa Wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi
kwa kutegemea posho wanazolipwa.
“Ni
vema ikaeleweka kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wote ni watu wenye
nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi
zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya
muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya”. Alisema
Mwakasyuka.
Mwakasyuka
ameongeza kuwa, si vema kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha Wajumbe
hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na
kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya Bunge Maalum vizuri kama
ilivyotarajiwa na wananchi.
Baadhi
ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wakisikiliza kjwa
makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey
Mwakasyuka wakati alipofanya mkutano na waandishi hao kwa lengo la
kutolea ufafanuzi kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini
Dodoma.(Picha zote na Benedict Liwenga-Maelezo).
Akifafanua
kuhusiana na malipo ya posho hizo, Mkurugenzi Mwakasyuka ameviambia
vyombo vya habari kuwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria
vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.
“Ni
vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za
umma na yanapita kwenye mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za
mahudhurio ya Wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina, na
upatikanaji wa fedha toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku
kadhaa hadi kukamilika.” Alifafanua Mwakasyuka.
Aidha,
Mwakasyuka amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyondika habari za
Bunge Maalum kuzingatia maadili na kanuni za Uandishi wa habari
zinazotolewa katika vikao vya Bunge Maalum ili taarifa kama hizo za
upotoshaji zisijirudie tena.
“Kumbukeni
kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata
kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini”. Alionya
Mwakasyuka.
Katika
kanuni za Bunge Maalum, kanuni ya 77 inawataka waaandishi wa habari
kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili
ya uandishi wa Habari ili kuondoa uandishi wenye kuleta chuki kati ya
Serikali na Wananchi wake kwani kinyume na kanuni hiyo, Katibu anaweza
wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa chombo chochote
cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za
Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au
vinginevyo inakiuka kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum.