Lampard Ajitia Kitanzi Kingine Man City

Kiungo kutoka nchini Uingereza, Frank James Lampard ameongeza mkataba wa kuitumikia klabu ya Man city, kutokana na matarajio ya Yaya Toure, kurejea nyumbani mwanzoni mwa mwaka 2015 kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika.

Lampard, ambaye aliifungia Man City bao la kujiokoa kutoka mikononi mwa Chelsea mwishoni mwa juma lililopita huko mjini Manchester alianza kufikiriwa kupewa mkataba mpya baada ya umuhimu wake kuonekana kwa kiasi kikubwa tangu alipojiunga na klabu hiyo kwa mkopo wakati wa maandalizi ya msimu.
Meneja wa Man City, Manuel Pellegrini alianza mapema kuusumbua uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha wanafanikisha mipango ya kumshawishi Lampard ili aweze kuendelea kuwa sehemu ya mipango yake.
Man city wana wigo wa kuendelea kumtumia Frank Lampard kwa mkopo wa zaidi ya miezi mitatu baada ya Januari, kutokana na ligi ya nchini Marekani kutarajia kuanza mwezi Machi mwaka 2015.
Ikumbukwe kwamba Frank Lampard alisajiliwa kwa mkopo na klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa nchini Uingereza, akitokea kwenye klabu ya New York City FC ya nchini Marekani na mkataba wa awali ulikuwa unaishia mwezi Disemba mwaka huu.
Katika kipindi ambacho Yaya Touye hatokuwepo Man City itakuwa inakabiliwa na michezo migumu dhidi ya Chelsea pamoja na Everton.

Popular Posts