Arsene Wenger Ni kiboko ya Mameneja 207 Wa Ligi Ya England Kwa Miaka 18

Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger hii leo ametimiza miaka 18 kamili tangu alipoanza kuitumikia klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London oktoba mosi mwaka 1996.

Wenger, anatimiza miaka 18 huku hii leo kikosi chake kikikabiliwa na mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Galatasaray kutoka nchini Urutuki ambapo itamlazimu kufanya jitihada za kuinogesha furaha ya kuwa klabuni hapo kwa muda mrefu kwa kikosi chake kusaka ushindi.
Uwepo wa meneja huyo kutoka nchini Ufaransa, unaendelea kumpa sifa ya tofauti katika ligi ya nchini Uingereza kutokana na kuwa mtu aliyedumu kibaruani kwa kipindi kirefu huku klabu nyingine zikifanya mabadiliko ya mara kwa mara katika mabenchi yao ya ufundi.
Tangu mwaka 1996 Arsene Wenger, akiwa meneja wa klabu ya Arsenal klabu nyingine 43 zilizoshiriki ligi tangu kipindi hicho zimebadilisha jumla ya mameneja 207 na kumuacha akiwa meneja pekee anaebaki kuwa kiongozi wa benchi la ufundi la The Gunners.
Kwa mantiki hiyo sasa Arsene Wenger, anaendelea kuwa meneja aliyedumu Arsenal kwa kipindi kirefu kuliko meneja mwingine yoyote aliyepita klabuni hapo na pia anakuwa meneja aliyekaa kwa kipindi kirefu zaidi ya wengine katika ligi ya nchini Uingereza baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson aliyekuwa akikinoa kikosi cha Man Utd.
Arsene Wenger alitambulishwa rasmi kuwa meneja wa klabu ya Arsenal Oktoba mosi mwaka 1996, baada ya kukamilisha mipangop ya kusaini mikataba na viongozi wa klabu hiyo Septemba 30 mwaka huo.

Popular Posts