Dawa ya kupaka ili kuzuia HIV haifai
Dawa iliokisiwa kupunguza uwezekano wa mwanamke kupata virusi vya HIV wakati wa tendo la ngono haifai,kulingana na utafiti mkubwa uliofanywa na shirika la Follow on Africa Consortium for Tenofovir kutoka Afrika kusini.
Matokeo ya utafiti huo unaojulikana kama facts 001 yalitolewa katika kongamano la magonjwa ya virusi na yale ya maambukizi nchini Marekani.
Kulingana na gazeti la mail and Guardian nchini Afrika kusini,wanawake katika utafti huo waliagizwa kujipaka dawa hiyo katika sehemu zao za siri kabla na kila baada ya tendo la ngono.
Matokeo hayo yanapinga matokeo ya utafiti mwengine uliochapishwa mwaka 2010 na shirika la mpango wa utafiti wa ugonjwa wa ukimwi nchini Afrika kusini Caprisa.
Watafiti waliwatumia zaidi ya wanawake 900 katika jimbo la Kwa Zulu Natal na kuripoti dawa hiyo ya Tenofivir ilikuwa na uwezo wa asilimia 39 pekee wa kupunguza viwango vya maambukizi ya viini vya HIV miongoni mwa wanawake hao.
Viwango vya maambukizi ya HIV nchini Afrika kusini vilikuwa asilimia 12.2 mwaka 2012 ikiwa ni vya juu zaidi duniani kulingana na utafiti wa baraza la sayansi ya binaadamu kuhusu kinga ya HIV ,visa na tabia.
Viwango hiyo ni vya juu miongoni mwa wanawake na kusababisha utafiti kutafuta tiba za kinga zinazowalenga wanawake kama vile dawa inayopakwa katika sehemu za siri,pamoja na sindano zilizojaa tiba za kukabiliana na HIV.
Wakati wa utafiti huo uliochukua takriban miaka mitatu,watafiti waliwatumia wanawake 2000 wasio na virusi vya ukimwi kati ya miaka 18 hadi 30, na kuwapatia nusu yao dawa ya Placebo na nusu nyengine wakapewa dawa ya kwenye sehemu za siri tenofivir,ambayo ni dawa ya kukabiliana na virusi vya ukimwi.
Baadaye watafiti walipima viwango vya maabumizi ya virusi vya HIV kati ya makundi mawili na kubaini kwamba wanawake waliopewa dawa hiyo ya Tenofivir waliambukizwa virusi vya ukimwi sambamba na wanawake waliopewa dawa kupaka ya placebo.
Kwa jumla wanawake 123 waliambukizwa virusi vya HIV huku 61 wakiwa ni wale waliopewa mafuta ya Tenofivir na 62 wakiwa walipewa mafuta ya placebo.