Ibrahimovic Kukosa Robo Fainali UEFA Imethibitika Rasmi


Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, limempunguzia adhabu mshambuliaji kutoka nchini Sweden, Zlatan Ibrahimovic ambaye alionyeshwa kadi nyekundu wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa ligi ya mabingwa barani humo dhidi ya Chelsea juma lililopita.

UEFA wametangaza mshambuliaji huyo wa klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya nchini Ufaransa ataukosa mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya robo fainali, mbali na michezo miwili kama ilivyotarajiwa na wengi kutokana na kanuni za michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Kamati ya nidhamu ya UEFA, imefafanua jambo hilo kwa kusema suala kubwa lililoangaliwa hadi kufikia hatua ya kupunguzwa kwa adhabu ya mshambuliaji huyo ni kufuatia kosa alilolifanya ambapo imebainika hakuwa na kusudio la kumchezea vibaya kiungo wa Chelsea, Oscar Emboaba Junior.
Katika hatua nyingine beki wa pembeni kutoka nyumbani Afrika katika nchi ya Ivory Coast, Serge Aurier amefungiwa kucheza michezo mitatu ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kubainika aliwatusi waamuzi kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Aurier, ambaye alikuwa majeruhi wakati wa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Chelsea aliandika ujumbe wa matusi katika mtandao wa kijamii ambao uliambatana na picha ya video ambapo alionekana akishangilia mara baada ya mchezo na kutoa maneno machafu dhidi ya waamuzi.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 22 alimlenga muamuzi kutoka nchini Uholanzi, Bjorn Kuipers aliyechezesha mchezo wa PSG dhidi ya Chelsea kutokana na ujumbe aliouandika na kuutamka kupitia Facebook.
Paris Saint-Germain hii leo watamfahamu mpinzani wao kufuatia shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kutarajia kupanga ratiba huko mjini Nyon nchini Uswiz.

Popular Posts