Skrtel wa Liverpool apigwa rungu
Mlinzi wa kilabu ya Liverpool Martin Skrtel atahudumia marufuku ya mechi tatu baada ya kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka nchini Uingereza FA kukataa ombi lake la kukata rufaa dhidi ya hatua ya kinidhamu dhidi yake.
Raia huyo wa Slovak alimkanyaga kipa wa Manchester United David de Gea katika dakika za lala salama za ushindi wa 2-1 wa Manchester United dhidi ya Liverpool katika uwanja wa Anfield siku ya jumapili.
Tukio hilo halikuonekana na refa Martin Atkinson.
Skrtel mwenye umri wa miaka 30 alisema kuwa kisa hicho hakikuwa cha makusudi.
Hatahivyo kamati hiyo ya nidhamu ilikataa ombi hilo hatua ambayo itamfanya mchezaji huyo kukosa mechi tatu za EPL huko Arsenal,Newcastle, pamoja na robo fainali ya kombe la FA dhidi ya Blackburn.