Akatazwa shule kwa kuvaa sketi ndefu
Msichana mmoja muislamu amekatazwa kuingia darasani huko shuleni kwao Ufaransa kwa sababu alikuwa amevalia sketi ndefu.
Msichana huyo mwenye umri wa 15 alifurushwa kutoka shuleni hapo na utawala wa shule hiyo uliodai amekiuka sheria za nchi hiyo zinazokataza kuonesha waziwazi ishara za kidini.
Kwa kawaida msichana huyo aitwae Sara, huvua hijabu yake anapokuwa maeneo ya shule kama inavyoamuriwa lakini hakudhani kwamba sketi yake ndefu pia ingemuweka matatani.
Ni mara ya pili Mkuu wa shule hiyo amemrudisha nyumbani mshichana huyo baada ya kumpa barua awapelekee wazazi wake inayoagiza kuwa abadilishiwe mavazi ndio aruhusiwe kuingia darasani. .
Inavyoelekea mgongano huu unatokana na tafsiri hiyo ya sheria ya 2004 inayozuia raia wa nchi hiyo kuonesha wazi wazi kuwa ni waumini wa dini fulani.
Msichana Sara anasema sketi yake si vazi la kidini, lakini utawala wa shule unatafrisi sketi hiyo yenye urefu wa hadi juu kidogo tu ya kisigino, kuwa vazi la kiislamu.