GIGGS ATACHUKUA NAFASI YANGU: VAN GAAL
Meneja wa Manchester United Louis van Gaal anadhani klabu hiyo itamteua Ryan Giggs kuchukua nafasi yake. Giggs alikuwa meneja wa muda na kusimamia mechi nne msimu uliopita baada ya David Moyes
kutimuliwa. Aliteuliwa kuwa meneja msaidizi wa Van Gaal mwezi Mey mwaka jana. Van Gaal, 63, anakaribia mwisho wa msimu wake wa kwanza na mkataba wake unakwenda hadi mwaka 2017. Alipoulizwa kuhusu Giggs, ameiambia TV ya Man United- MUTV: "Natarajia kuwa atakuwa meneja mimi nitakapoondoka." Ameongeza kusema: "Sasa mimi nina majukumu yote. Yeye ana jukumu kama la wachezaji. Kila anachokifanya kwangu mimi anakifanya vyema sana." Giggs, 41, amesema ulikuwa "muda wa kujivunia" katika fani yake wakati alipokuwa meneja wa muda, kufuatia kufukuzwa kwa Moyes. Giggs, aliyeichezea Manchester United mara 963, alishinda mechi mbili, kutoka sare moja na kupoteza mechi moja, wakati akiwa meneja wa muda.