Hassan Kessy aiwekea ngumu Simba
Kessy ameshindwa kuondoka na timu kutokana na uongozi wa timu kutommalizia pesa zake za usajili Sh 15 Milion pamoja na nyumba ya kuishi
BEKI wa kulia wa Simba Hassan Kessy ameshindwa kuondoka na timu yake kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya pambano la Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar, kutokana na uongozi wa timu hiyo kutommalizia pesa zake za usajili Sh 15 Milion pamoja na nyumba ya kuishi.
Hassan Kessy 22, aliyejiunga na Simba kwenye usajili mdogo akitokea mtibwa Sugar ameiambia Goal, kwa sasa yupo kwao Morogoro na atarudi kuendelea na kazi yake wakati uongozi wa timu hiyo utakapomlipa stahiki zake ambazo ni fedha na kumpa nyumba ya kuishi.
“Nimeamua kurudi nyumbani Morogoro kwasababu viongozi wa Simba wamekuwa wakinidanganya kila ninapowauliza kuhusu haki yangu namuda ndio unakwenda ligi inakaribia kumalizika,”amesema Kessy’
Msemaji wa Simba Haji Manara ameiambia Goal, Kessy hayupo kwenye kikosi kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini alipobanwa zaidi akasema hakuna mtu anayejua mkataba wa Kessy na Simba ukoje hivyo inawezekana malalamiko yake hayapo kwenye mkataba.
Kocha Goran Kopunovic atalazimika kukosa huduma ya nyota huyo Jumamosi watakapokuwa ugenini kwenye uwanja wa CCM Kambarage, kuwakabili Kagera Sugar na sasa nafasi hiyo huenda ikatumiwa na Nassor Masoud Chollo au William Lucian ‘Gallas’