Mashali: Sitaki Kusikia Masumbwi Katika Maisha Yangu



Bondia Thomas Mashali, ametangaza kuachana na mchezo wa masumbwi baada ya kuibuka kwa mtafaruku baina yake na viongozi wa mashirikisho ya ndondi ya kulipwa hapa nchini kutokana na kushindwa kupanda ulingoni mwishoni mwa juma lililopita kumkabili Karama Nyilawira.

Mashali ametangaza kujiondoa katika mchezo huo, kwa madai ya viongozi na mapromota kutokua na moyo wa kibinaadam dhidi yake kutokana na kutambua matatizo ya kiafya yaliyokua yakimsumbua kabla ya mpambano wake dhidi ya Nyilawira.
timesfm.co.tz imefanya mahojiano na bondia huyo, ambapo alisema kwa sasa anafikiria kufanya jambo lingine, ambalo litamuendeshea maisha yake na anaamini mabondia anaowaacha ulingoni wana uwezo wa kupambana na kuuendeleza mchezo wa masumbwi nchini Tanzania.
“Kwa sasa nawaachia mabondia kama Japhet Kasseba, Mada Mauhugo na wengine ili waendelee na mchezo huo lakini kwangu ninaona nimefika mwisho kutokana na sababu ambazo zimenikwaza”.
Sababu zilizooelezwa na Mashali ambazo zimemsababishia maamuzi ya kujiweka pembeni na mchezo wa masumbwi, alidai kwamba viongozi na mapromota wamekua na moyo wa kinyama bila kujali ubinaadamu wa mabondia.
Bondia huyo alisema kuwa kabla ya pambano lake na Karama Nyilawira alikutana na viongozi wa mashirikisho ya ngumi za kulipwa TPBO pamoja na PST na kuwaambia anaumwa jicho, lakini hawakuonyesha kumjali.
Pia alidai kwamba taarifa hizo alizifikisha kwa Promota Jay Msangi, lakini bado hakusikilizwa na badala yake alilazimishwa kwenda kupima uzito tayari kwa pambano lake la ijumaa dhidi ya Karama.
“Ndugu yangu watu wamekosa ubinaadamu na hawatujali kabisa sisi mabondia hali hii imenisikitisha sana na sioni sababu ya kuendelea na mchezo huu, kutokana na mambo yanavyopelekwa”.
“Kuanzia sasa sitakia kabisa kusikia habari za mchezo wa ngumi, na sitokua tayari kuzungumza na chombo chochote cha habari kuhusiana na mchezo huu, kama kuna mambo mengine nitazungumza lakini sio ngumi”. Alisema Mashali
Mashali alisisitiza kufanya maamuzi hayo bila kushurutishwa na mtu yoyote na aliutaka umma wa mashabiki wa masumbwi kuheshimu alichokiamua.

Popular Posts