Timu ya Yanga yatwaa ubingwa ligi kuu ya Tanzania 2014/2015
Timu ya Yanga wamekuwa mabingwa wapya wa ligi kuu ya Tanzania kwa mwaka 2014/2015 na hivyo kuivua rasmi ubingwa Azam iliyokuwa ikishikilia taji hilo.
Ubingwa wa Yanga unakuja baada ya kuizamisha timu ya Polisi Morogoro kwa jumla ya mabao 4-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jumatatu, jijini Dar es Salaam, ilikuwa inahitaji ushindi wa pointi tatu kutangazwa bingwa mpya ikibakiwa na michezo miwili mbele.
Kabla ya mchezo huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa pointi 52 ambapo sasa imefikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ya ligi hiyo ya Vodacom.
Azam ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 kwa sasa, endapo itashinda michezo yake iliyobaki itafikisha pointi 54 tu.
Vita ya kusaka nafasi ya pili sasa imebaki kwa Azam na Simba iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 41.
Timu za Prisons, Polisi na Ndanda ziko hatarini kushuka daraja.
Timu 14 zinashiriki ligi kuu ya Vodacom nchini Tanzania.