Wasomali walalama kufungwa kwa Hawala Kenya
Jamii ya wasomali nchini Kenya wamelalamikia vikali hatua ya serikali nchini humo kufunga mashirika kumi na tatu ya ubadilishaji wa sarafu za kigeni na usafirishaji pesa maarufu kama Hawala.
Malalamishi yao ni kuwa hatua hiyo itasababisha matatizo makubwa kwa wasomali ambao daima wanategemea njia hiyo, kuwatumia jamaa zao fedha kutoka mataifa ya kigeni.
Hatua hiyo imefanyika baada ya shambulio la Al-Shaabab katika Chuo kikuu mjini Garrisa juma lililopita.
Serikali ya Uhuru Kenyatta inasema kuwa ni mojawepo ya njia ya kuzuia al-Shabaab kupata fedha ili kupanga na kutekeleza mashambulio zaidi.
Hali ya hatari ya kutotembea nje usiku pia imewekwa katika majimbo yaliyo na wasomali wengi kazkazini mashariki mwa Kenya.
Akaunti za Benki za watu themanini na sita zinazodhaniwa kufadhili ugaidi pia zimesitisha.
Gavana wa benki mkuu ya Somalia Bashir Issa Ali ameiambia shirika la habari la Reuters amethibitisha kuwa amepokea ilani hiyo kutoka kwa benki kuu ya Kenya.
Waziri wa maswala ya kigeni wa Kenya Amina Mohamed amesema kuwa nchi yake imeomba msaada wa kijasusi kutoka mataifa ya magharibi
kufuatia shambulizi baya zaidi katika miaka ya hivi punde iliyosababisha vifo vya watu 148 wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Garissa.