Uzinduzi wa Windows 10 ni mwanzo mpya
Programu ya Windows 10 imeadhimisha
mwanzo mpya katika kompyuta za kibinafsi ,kulingana na mtendaji mkuu wa
kampuni ya Microsoft .
Programu hiyo ilizinduliwa kimataifa siku ya Jumatano, na ni jaribio la kampuni hiyo kujaribu bahati yake katika sekta ya simu.
Windows 10 itatolewa bure kwa wateja wengi kama hatua ya kuboresha programu hiyo.
Hata hivyo makampuni yatalazimka kulipia toleo hilo jipya hivyo watengenezaji wa PC watahitajika kuiweka katika vifaa hivyo.
Wachambuzi wanasema mkakati huo umezinduliwa ili kuharakisha utumizi wake.
Alipofanya mazungumzo ya kipekee na BBC, Satya Nadella alisema ''programu ya windows 10 ni hatua kubwa kwetu sisi kama kampuni, na katika sekta nzima''.
Microsoft imekua mbioni kuizindua kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita, hivyo si kila mtu atapata fursa hiyo ya kuboreshewa siku ya kuanzishwa kwake.