Makanisa mengine manne yachomwa mkoani kagera
Makanisa manne yameteketezwa katika mkoa wa Kagera, kaskazini magharibi mwa Tanzania na kufikisha saba, idadi ya makanisa yaliyochomwa moto eneo hilo mwezi huu.
Hadi sasa haijabainika ni kundi gani linalohusika na vitendo hivyo, kwa mujibu wa polisi.
Lakini baadhi ya viongozi wa dini wameambia mwandishi wa BBC Leonard Mubali kuwa huenda ni matokeo ya uhasama wa kidini.
Kuchomwa kwa makanisa hayo kumeongeza hofu kwa viongozi wa makanisa na waumini kuhusu usalama wao.
Mchungaji Vedasto Athanasi ni Askofu wa kanisa la Living Water mkoani humo, ambaye kanisa lake limechomwa kwa mara ya tatu sasa, ni mmoja wa walioingiwa na wasiwasi.
“Kitendo hakiwezi kukafanyika mara tatu, na hakuna hatua zinazochukuliwa. Naona ufuatiliaji wa suala hili ni mdogo sana,” amesema.
Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongela, ameiambia BBC kuwa mazingira ya matukio hayo yana utata kiasi kwamba ni vigumu kutambua mara moja kuwa yana malengo gani.
”Kwa jinsi ambavyo tuliona, hupati shida ya moja kwa moja, ujue kama ni siasa au ni nini. Kwa sababu haya yanafanyika wakati hakuna watu,” amesema.
”Lolote lile ambalo litakuja upande wetu, tutalifanyia kazi na kuona kama litatusaidia katika kutuelekeza.”
Crodward Edward, mwenyekiti wa muungano wa makanisa ya Kipentekoste mkoani Kagera, anasema anaridhishwa na hatua za mamlaka za usalama na kuwataka waumini kuwa watulivu kipindi hiki cha matukio haya.