Utamuokoa nani, mamako ama mpenzi wako?

Ungelazimishwa kuamua nani utakayemuokoa, ungemuokoa mamako au mpenzi wako kutoka kwa jumba linaloteketea?
Hili ni swali tata linaloulizwa sana Uchina. Na mwaka huu, lilikuwa kwenye mtihani wa kitaifa wa uanasheria, likiulizwa mawakili na majaji wa siku za usoni.
Wanaopita mtihani huo ndio pekee huruhusiwa kuhudumu kama wanasheria nchini Uchina.
Wajua jibu sahihi lilikuwa gani? Wizara ya Haki nchini Uchina baadaye ilichapisha jibu “sahihi”: kwamba watahiniwa wana wajibu wa kuwaokoa mama zao. Litakuwa “kosa la kutochukua hatua” kwa mtu kuamua mapenzi kwanza badala ya damu.
Lakini jibu hilo si rahisi sana kwa watumiaji wa mtandao Uchina, ambao wamekuwa wakijibizana kuhusu jibu sahihi. “Ni jambo la kushangaza kulinganisha jukumu la kuwasaidia wazazi na jukumu la kusaidia wengine wakati wa dharura,” alilalamika mmoja.
“Kwa mujibu wa sharia, mwana wa kiume lazima amuokoe mamake,” alilalamika mwingine. “Lakini sharia haisemi lazima amuokoe mamake iwapo kuna watu wengine ambao wamo hatarini pia.”
Wengine walipoulizwa wangemuokoa nani, penzi la mama lilionekana kuongoza. “Wasichana wamejaa kila pahali, lakini nina mama mmoja pekee,” kijana mmoja alisema. “Bila shaka ningemuokoa mamangu kwanza,” alisema mwingine. “Kando na sababu za kisheria, mamangu alinilea. Isitoshe, mpenzi wangu ni mchanga, na ina maana kwamba ana uwezekano wa juu kujiokoa bila usaidizi”
Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna yeyote mtandaoni Uchina aliyeonekana kugundua mwegemeo wa kijinsia wa swali hilo. Labda kungelikuwa na swali la ni nani mwanamke anayefaa kumuokoa kwanza, babake au mvulana mpenzi wake.

Popular Posts